Wednesday, September 14, 2016

Mjadala: Uchumi Wetu Unaweza Kuhimili Mabadiliko ya Rais Magufuli?

 
Na. M. M. Mwanakijiji

Habari kubwa wiki hii inayoisha ni kuwa viashiria mbalimbali vya uchumi – japo siyo vyote – vinaonesha kuwa uchumi wetu unaelekea kupooza kwa kiasi na hili limewafanya baadhi ya watu kuanza kutabiri kuzimika kabisa kwa uchumi wetu. Inawezekana kabisa kuwa zipo sababu za msingi za kuzungumzia hali ya uchumi lakini siamini kuwa sauti tunazozisikia sasa hivi zote zinasema hivyo kwa sababu zinaamini kweli kuwa hali ya uchumi imefikia pabaya kiasi hicho.


Hofu kubwa ambayo ninayo ni kuwa katika kuangalia mambo mazito kama haya ya uchumi takwimu zinaweza kutumika vyovyote vile. Msomi mmoja William W. Watt aliwahi kusema kuwa “usiweke imani katika kile ambacho takwimu zinasema hadi pale utakapoona kile ambazo hazisemi”. Ni rahisi sana kunukuu baadhi ya takwimu na ukasema lolote juu yake.

Hili tumeliona na wakati mwingine nahofia kuwa wasomi wanatumia takwimu hizi kujaribu kujenga hoja Fulani na hivyo kwa makusudi – siyo kwa bahati mbaya – wataacha pembeni takwimu zozote zile ambazo labda hazielezei au haziendani na ile hoja yao ya mwanzo. Kwa wale ambao wanaamini kuna kudorora kwa uchumi basi wataenda na tumeona wameshaenda kutafuta takwimu zozote zile ambazo zinaonesha hili na wakaweka pembeni takwimu nyingine zozote zinazokinzana na hizo.

Mojawapo ya makosa makubwa yanayotokea katika ujengaji hoja wa kimantiki (logical fallacies) ni ile ambayo inajaribu kuonesha kuwa kwa vile vitu fulani vimetokea wakati ule ule au kwa ukaribu fulani basi vitu hivyo vinahusiana kama chanzo na matokeo. Ndugu zetu ambao wametuambia kuhusu takwimu mbalimbali za kiuchumi kama zilivyo kwenye tovuti ya BoT wanataka kutuambia kuwa takwimu hizo ni ‘matokeo’ ya hatua fulani fulani zilizochukuliwa na Serikali ya Magufuli.

Siyo kusudio langu hasa kuzungumzia madai haya mbalimbali ambayo ni rahisi kuyachambua na kuyaonesha ni jinsi gani hayana msingi bali kusudio langu ni kujaribu kuhoji uwezekano na maoni yangu ya nini matokeo ya uwezekano wa uchumi wetu kuguswa na maamuzi ya kisiasa. Ni rahisi baada ya muda na utafiti wa kutosha kuweza kuonesha ni jinsi gani viashiria mbalimbali vya uchumi vinahusiana na maamuzi mbalimbali ya kisera au kiutendaji ambayo tayari yamechukuliwa au yatachukuliwa.

Swali langu hata hivyo ni la kinadharia; je, inawezekana hatua mbalimbali za kisera, kiutendaji, na kisheria ambazo zinachukuliwa zinaweza kuathiri uchumi wetu; na je, uchumi wetu unaweza kuhimili mshtuko huo?[​IMG]

Jambo la kwanza ambalo naamini linahitaji kuangaliwa ili kuweza kujua au kukisia matokeo ya maamuzi hayo mbalimbali ni je Tanzania ilikuwa imefikia wapi katika miaka hii yote ambayo tumekuwa tukipiga vita dhidi ya ufisadi? Vigezo mbalimbali vinavyokubalika vya kimataifa vinaionesha Tanzania kuwa ni miongoni mwa nchi ambazo ufisadi unaonekana katika hali ya juu na hali ya maendeleo ya watu ikiwa chini. Mojawapo ya taasisi zinazofuatilia mambo ya ufisadi ya GAN inaonesha (ikitumia taarifa mbalimbali) jinsi gani ufisadi katika aina zake mbalimbali ulikuwa umezama katika jamii yetu. Kuanzia manunuzi ya umma, masuala ya ardhi, mahakama, polisi, n.k

Kiasi kwamba, ufisadi ulikuwa ni kama sehemu fulani ya maisha; na wengine tumewahi kuita pia ni aina ya sekta isiyo rasmi lakini yenye nguvu kubwa sana. Wapo wasomi ambao wamewahi kuonesha katika taarifa zao jinsi gani ufisadi kwenye baadhi ya nchi ambazo vyombo vyake vya utawala ni dhaifu unaweza kuwa ni sehemu ya namna ya kuendesha uchumi wan chi kabisa. Ukitembelea tovoti ya World Economic Forum na kuangalia takwimu mbalimbali unaweza kukubaliana name kuwa pamoja na mafanikio mbalimbali ambayo tumeyaona miaka hii kumi na tano hivi iliyopita bado kama taifa kuna changamoto kubwa.

Swali ni kwa kiasi gani mafanikio hayo – kama tunaweza kuyaita mafanikio – yanahusiana na ufisadi mkubwa uliotokea miaka hiyo hiyo kumi na tano hivi? Je, kuna uhusiano wowote wa kuongezeka kwa vitendo vya ufisadi mkubwa na kuinuka kwa hali ya uchumi, pato la taifa n.k? Na kinyume cha hili ni kwa kiasi gani kuudhibiti ufisadi kweli kweli kunaweza kukawa na matokeo katika uchumi na matokeo yenyewe yakawa hasi kwa muda fulani?

Binafsi ninaamini – kwa kuangalia viashiria mbalimbali na siyo vya muda tu mfupi kama wenzangu wanavyofanya – uchumi wa Tanzania ulipaswa na ulitakiwa uoneshe kuguswa na maamuzi ya kudhibiti ufisadi, kusimamia utawala wa sheria, kuboresha au kufanya mabadiliko katika mfumo wa kodi n.k Ni sawasawa na ujio wa tetemeko; majengo yaliyojengwa vibaya au yasiyozingatia uwezekano wa tetemeko yataathirika zaidi na tetemeko kulinganisha na majengo ambayo yamejengwa kuhimili matetemeko ya ardhi.

Je, uchumi wetu ulivyo ulijengwa kuweza kuhimili misuko suko ya kiuchumi? Inawezekana kwa muda tuliweza kuhimili misukosuko ya kawaida ya kiuchumi kama kupanda kwa bei ya mafuta, matatizo kwenye taasisi za fedha, ukame n.k lakini sidhani kama kifikra tulijiandaa kufikiria kuwa ufisadi katika aina zake mbalimbali ukidhibitiwa kwa ghafla kutakuwa na matokeo gani kwa nchi na kwa taifa.

Naomba kupendekeza kuwa pamoja na sababu nyingine inawezekana kabisa kuwa haya tunayoyaona katika uchumi na katika hali zetu mbalimbali ni hali ya mpito. Ni hali ya mpito kwa sababu siyo tu yalitakiwa kutokea bali pia yalipaswa kutokea; kwani kama yasingetokea sijui tungejua vipi kuwa hali ilikuwa mbaya sana? Ni kama mgonjwa ambaye amepelekwa chumba cha upasuaji akiwa mahututi akiamka na kukuta hajapasuliwa si atahoji nini kimetokea? Lakini akikuta anakidonda na anaangaliwa na wauguzi hata kama hatoweza kuamka saa ile ile lakini atakuwa na uhakika kuwa baada ya muda nguvu na afya itamrejea.

Hivyo ndivyo ilivyo. Ni kweli inawezekana kuwa tukaona hali ngumu, na maisha magumu kwa wakati huu lakini haya yote yalipaswa kuwepo. Na hili lisichukuliwe kama Magufuli “hajali” au “ana roho mbaya”. Kitu pekee ambacho binafsi ningeogopa ni kama Magufuli asingeanza kuchukua hizi hatua mbalimbali za kumponya mgonjwa. Na kama nitakavyoonesha wiki ijayo –ikimpendeza Mungu – bado hajaenda mbali zaidi katika hatua za kuliponya taifa kama baadhi yetu tulitarajia. Kuna hatua ambazo binafsi niliamini zilipaswa ziwe zimeshakuliwa hadi hivi sasa lakini hazijachukuliwa na hata katika hatua zilizochukuliwa bado kuna mengine ambayo hajayafanywa na hili linatoa mwanya kwa mafisadi kuendelea kupeta.

Tulipofika sasa hivi tusikate tamaa, tusirudi nyuma na wala tusife moyo kwani uchumi wetu utatulia, na baadaye utaanza kweli kuendeshwa kwa kiasi kikubwa kabisa kwa shughuli halali za uzalishaji mali na huduma mbalimbali. Kwamba itakuwa nchi ambayo ufisadi mkubwa na ule mdogo mdogo utakuwa umedhibitiwa kwa kiasi kikubwa na hivyo kutoa nafasi nzuri kwa kile anayetaka kujaribu ndoto yake kuwa na angalau nafasi sawa katika uwanja wa ushindani kuliko ilivyokuwa huko nyuma.

Tukiona tunaletewa takwimu tusiwe na haraka ya kukubali tu au kupinga kwani kama mtu mmoja alivyowahi kusema huko nyuma, takwimu ni kama nguo za kina dada kuogelea, zinaonesha kile cha kishawishi tu lakini zinaficha kilicho muhimu kabisa.

0 comments:

Post a Comment