Friday, September 16, 2016

Wabunge wote wa CUF Wamkataa Profesa Ibrahim Lipumba


Wabunge wote wa Chama cha Wananchi (CUF) wametangaza rasmi kutomtambua aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.

Wamemtaka Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi kutomkumbatia mwanasiasa huyo aliyebobea katika uchumi, ikielezwa kwa sasa hana sifa za kuwa mwenyekiti wa chama hicho, labda aanze upya mchakato.

Wameeleza msimamo huo jana mjini Dodoma na Mbunge wa Viti Maalumu, Riziki Mngwali ambaye pia ni Kiongozi wa Wabunge wa CUF katika mkutano baina ya waandishi wa habari za Bunge na wabunge wa CUF isipokuwa Mbunge wa Jimbo la Kaliua, Magdalena Sakaya aliyesimamishwa uanachama, ingawa anaendelea kutimiza majukumu yake bungeni.

Mngwali alisema Profesa Lipumba amekuwa akijaribu kukiyumbisha chama na hivi karibuni kudai amekaririwa akisema anasubiri barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa ya kuthibitishiwa kuendelea na uenyekiti wake.

“Wakati anajiuzulu uenyekiti Agosti 5, mwaka jana aliutangazia umma na kudai anakwenda Rwanda kwa kazi aliyodai ya utafiti ili aje kuisaidia serikali, lakini inashangaza sasa anataka kujirejeshea uenyekiti. Hilo hatukubali kwa kuwa chama kina taratibu zake,” alisema.

Aliongeza kuwa, alikiacha chama katika wakati mgumu kuelekea Uchaguzi Mkuu, lakini kikaimarika zaidi kwa kupata wabunge 43, madiwani 287, kuongoza manispaa mbili na halmashauri za wilaya tatu, hivyo wanashangazwa kuona akitaka kurejea, tena kwa kutumia nguvu.

“Tunataka ifahamike kwa dhati kuwa, sisi wabunge, hatumtambui tena Profesa Lipumba kama Mwenyekiti wa CUF,” alisema Mngwali na kumtaka Msajili kutomuidhinisha Lipumba, kitendo alichodai kitachochea mgogoro ndani ya chama.

Aliongeza kuwa badala ya kutumia mabavu kutaka kurejea madarakani, ni vyema akabaki na heshima yake, kwani amekitendea mambo mengi chama hicho na kwamba wanamheshimu, hivyo afuate taratibu za kichama kutaka kuwania tena uenyekiti.

Mngwali alisema wamekubaliana na uamuzi wa Baraza Kuu la Uongozi wa CUF wa kuwasimamisha uanachama Lipumba na wenzake tangu Agosti 28, 2016 kutokana na kile kinachodaiwa kukiuka Katiba ya chama hicho. 

Miongoni mwa tuhuma zao ni kusababisha vurugu wakati wa Mkutano Mkuu Maalumu wa Uchaguzi Agosti 21, mwaka huu jijini Dar es Salaam uliokuwa unalenga kumthibitisha Juma Duni Haji kuwa Mwenyekiti mpya.

Hata hivyo, kutokana na vurugu zilizoibuka, mkutano huo ulivunjika. Mbali ya Lipumba na Sakaya, wengine waliositishiwa uanachama ni Abdul Kambaya ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, Ashura Mustapha, Omar Mhina, Thomas Malima, Kapasha M. Kapasha, Mohamed Habib Mnyaa, Haroub Shamis na Mussa Haji Kombo.

Ashura ni mjumbe wa Baraza Kuu na aliwahi kuwa Naibu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano ya Umma CUF wakati Mnyaa na Kombo, walikuwa wabunge kipindi cha 2010/2015, Mnyaa akiwakilisha Jimbo la Mkanyageni na Kombo Jimbo la Chake Chake, kisiwani Pemba.

Kutokana na kusimamishwa kwa viongozi hao, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui alimtangaza Julius Mtatiro aliyewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu Bara kuwa kiongozi wa Kamati ya Uongozi wa muda inayowajumuisha pia wabunge Katani Ahmed Katani na Savelina Mwijage ambao ni wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa.

0 comments:

Post a Comment