IDADI kubwa ya watu inasumbuliwa na tatizo la kuwashwa sehemu za siri bila kujali jinsia na umri.
Watu
wengi wanaamini kuwashwa sehemu za siri kunasababishwa na fangasi tu,
ndiyo maana nimepata maswali ya wasomaji juu ya matibabu na jinsi ya
kujikinga na fangasi kwa kuwa wanaamini muwasho unaowasumbua kwa muda
mrefu ni matokeo ya maambukizi ya fangasi.
Watu
wanapaswa kufahamu kuwashwa sehemu za siri kunaweza kuwa dalili ya
maradhi fulani ndani ya mwili wako pengine isiwe ni fangasi na ikawa ni
mzio (allergy) tu.
Mara
nyingi muwasho sehemu za siri unaosababishwa na kitu huisha wenyewe
kitu hicho kikiondolewa. Kuondolewa kwa kitu hicho kunatia ndani
matibabu sahihi na kuendelea na njia bora za kujikinga kutopata
maambukizi tena. Vitu vingine vinavyosababisha muwasho huhitaji matibabu
ya hali ya juu zaidi. Ikiwa unawashwa kwa muda mrefu ni vyema
kuzungumza na daktari. Kukaa na ugonjwa kwa muda mrefu kunaweza
sababisha ugonjwa kusambaa mwilini na kuongeza hatari ya kifo.
Nini husababisha Muwasho Sehemu za Siri za Mwanaume?
Kuwashwa
uume au sehemu zingine za siri za mwanaume husababishwa na sababu zile
zile zinazosababisha muwasho sehemu nyingine za mwili.
Maradhi
ya fangasi husababisha muwasho kwa wanaume wengi, sababu nyingine ni
kama ugonjwa wa upele (scabies), kuwepo kwa chawa, mzio na maambukizi
mengine ya bakteria. Maambukizi hasa ya magonjwa ya zinaa ndio chanzo
kikuu cha kuwashwa uume.
Fangasi sehemu za siri za mwanaume ni nini?
Maradhi
ya fangasi (Candidiasis) husababishwa na vimelea viitwavyo Candida
albicans. Vimelea hivi hushambulia jinsia zote ingawa hushambulia sana
jinsia ya kike kutokana na maumbile yao ya sehemu za siri kuwa na
unyevunyevu kitu kinachosababia wao kuathiriwa zaidi.
Watu
wengi wana vimelea hivi katika miili yao kwa kiwango kidogo sana. Kinga
ya mwili ikisaidiwa na bakteria walinzi wa mwili huweza kupambana na
vimelea hivi.
Mwanaume anapataje fangasi sehemu za siri?
Mtu
anapokunywa dawa za kuua bakteria kutokana na ugonjwa mwingine wa
bakteria kama kuhara damu, husababisha bakteria walinzi wa mwili kufa,
hivyo kuongeza hatari ya mwili kushambuliwa na ugonjwa wa fangasi.
Ikiwa
kinga yako ya mwili itashuka kutokana na maradhi kama VVU/UKIMWI au
lishe duni pia mwili wako utakuwa katika hatari zaidi ya kupata maradhi
ya fangasi.
Hata
hivyo, maradhi ya fangasi yanaweza kutoka kwa mtu mmoja hadi kwa
mwingine kwa kuchangia nguo au vifaa vya kuogea na kujamiana na mtu
mwenye ugonjwa wa fangasi.
Wanaume
wengi wanaosumbuliwa na fangasi sehemu za siri huishi maeneo yenye joto
sana kama Pwani, Lindi, Mtwara, Tanga na Dar es salaam.
Kuishi
sehemu yenye joto pamoja na kuvaa nguo za kubana hasa zisizo tengenezwa
na pamba kwa asilimia 100 kunafanya sehemu za siri kuwa na unyevunyevu,
hivyo kutengeneza mazingira mazuri kwa fangasi kuzaliana na kuongezeka.
Dalili za fangasi sehemu za siri za mwanaume ni zipi?
Sehemu
za siri za mwanaume hata ndani ya uume, korodani, eneo katikati ya
makalio na kuzunguka korodani hadi kwenye mapaja huathirika na ugonjwa
wa fangasi.
Kichwa
cha uume hubadilika na kuwa chekundu na kuwasha. Ngozi inayozunguka
sehemu za siri huwasha, kukakamaa na kutoa majimaji ambayo hutoa harufu
mbaya.
Matibabu ya fangasi sehemu za siri za mwanaume ni yapi?
Ikiwa una dalili za ugonjwa wa fangasi ni vyema kufika kwa daktari kwa ajili ya matibabu na ushauri zaidi.
Kutumia
dawa bila ushauri wa daktari kunaweza sababisha kutopona kabisa,
kutopona vizuri au ugonjwa kujirudia baada ya siku chache, pia vimelea
vinaweza kujenga usugu wa dawa.
Kumwona daktari kutasaidia kujua kama una maradhi mengine yanayosababisha upate fangasi sehemu za siri.
Ugonjwa wa fangasi usipotibiwa husambaa kwenye damu na kusababisha madhara makubwa mwilini kama kwenye ubongo na mapafu.
Mwanaume atajikinga vipi na fangasi sehemu za siri?
Ili
kusaidia kuepuka kupatwa na fangasi sehemu za siri ni vyema kuosha
vizuri uume, na kwa wale ambao hawajatahiriwa wanapaswa kuosha kwa
umakini zaidi hadi sehemu za ndani za govi.
Ziweke
sehemu zako za siri pamoja na ndani makalio katika hali ya usafi na
ukavu, kwa maana unyevunyevu unaweza sababisha maambukizi.
Matumizi ya poda maalumu yanaruhusiwa hasa kipindi cha joto kali ili kuzuia unyevunyevu.
Vaa
nguo isiyobana sana, iliyotengenezwa kwa vitu asilia kama pamba. Badili
nguo ya ndani (chupi) angalau kila siku na vaa kondomu kila unapofanya
ngono na mwanamke usiyejua hali yake kiafya kwa ujumla.
Saturday, September 17, 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment