Mahakama Kuu ya Tanzania, Kitengo cha Ardhi, imetupilia mbali pingamizi
lililowekwa na mawakili wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), katika kesi
iliyofunguliwa na Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema).
Awali, mawakili wa NHC walidai kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa
kusikiliza shauri hilo na kwamba mkataba baina ya Mbowe na NHC juu ya
umiliki wa jengo la Bilcanas lililopo mtaa wa Makunganya jijini Dar es
Salaam umeisha.
Upande wa utetezi ukiongozwa na wakili Peter kibatala ulidai kuwa,
mahakama hiyo ina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, hivyo inaweza ikatoa
uamuzi wowote na ndiyo maana wamewasilisha maombi hayo ili yatolewe
uamuzi.
Akitoa uamuzi wa pingamizi la mawakili wa NHC jana, baada ya kuwa
amesikiliza hoja za mawakili wa pande zote mbili, Jaji Siyovelwa
Mwangasi alisema kuwa hoja za Mawakili wa NHC hazina mashiko kisheria
kwani suala la mkataba wa umiliki Jengo hilo linahitaji ushahidi.
Jaji Mwangasi alisisitiza kuwa zuio la NHC kutopiga mnada mali za Mbowe,
lilizozichukua wiki mbili zilizopita kupitia mawakala wa kampuni ya
Fosters Auctioneers katika ukumbi wa Bilcanas na katika ofisi za kampuni
ya Free Media lipo pale pele.
Shirika hilo linamtuhumu Mbowe kutolipa deni la Sh. 1.3 bilioni, ikiwa
ni jumla ya fedha za kodi ya kupangishwa kwenye jengo hilo huku Mbowe
akifungua kesi katika Mahakama Kuu, Kitengo cha Ardhi, kupinga madai
hayo ya NHC.
Katika kesi hiyo namba 722 ya mwaka 2016, Mbowe anawakilishwa na
Mawakili na Peter Kibatala na Omary Msemo ilihali NHC ikiwakilishwa na
mawakili wake Aloyce Sekule na Miriam Mungula.
Katika hoja zake Mbowe anadai kuwa, yeye na shirika hilo walikubaliana
kwamba alikarabati na kulipanua jengo hilo kwa gharama zake kwa asilimia
100, makubaliano ambayo waliyaingia mwaka 1997.
Katika makubaliano hayo, Mbowe amedai kuwa walikubaliana kumiliki jengo
hilo kwa pamoja kwa muda wa miaka 99, huku yeye akitakiwa kupata
asilimia 75 katika mgawanyo wa mapato na NHC ikitakiwa kupata asilimia
25.
Hivyo amedai kuwa hatua ya NHC kumtoa kwenye jengo na kuchukua mali zake
ni kuvunja mkataba huo. Mbowe aliondolewa kwenye jengo hilo mnamo
Septemba Mosi mwaka huu.
Baada ya mahakama kufanyia uamuzi pingamizi lililowekwa na mawakili wa
NHC, kesi hiyo imeahirishwa mpaka tarehe 27 Septemba, mwaka huu ambapo
itaanza kusikilizwa rasmi.
Saturday, September 17, 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment