Tanzania imetajwa kuwa nchi ya kwanza duniani kufanikiwa katika utoaji wa huduma za kifedha kwa kutumia mitandao ya simu.
Hayo yameelezwa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka
ya Mawasiliano Nchini (TCRA) Eng. James Kilaba katika mkutano wa
kimataifa wa wadau wa mawasiliano ulioandaliwa na Shirika la Kimataifa
la Mawasiliano (ITU) kwa kushirikiana na TCRA pamoja na Benki Kuu ya
Tanzania (BOT).
“Huduma za kifedha kwa mfumo wa digitali nchini Tanzania imepiga hatua
kubwa ,ni nchi ya kwanza tuseme ulimwenguni kwa kutuma fedha na kutoa
kwa njia ya simu bila matatizo yoyote, pia kuna mfumo wa kutuma fedha
benki kwa kutumia mitandao ya simu,” alisema.
Kuhusu mkutano huo wa kimataifa ulioshirikisha washiriki zaidi ya 150
kutoka nchi mbalimbali duniani ambazo ni wanachama wa ITU, alisema
umelenga kujadili namna ya kufikisha huduma za kifedha kwa njia ya simu
katika sehemu ambazo hazifikiwi na huduma hiyo.
“Mkutano huu unasimamiwa na shirika la mawasiliano duniani ITC ambao
umelenga kujadili namna ya kutumia mitandao ya simu kupeleka huduma za
kifedha katika maeneo yasiyofikiwa na huduma za kifedha hasa ambako
hakuna mabenki. Mkutano huu nchi imeamua kuuanda kwa ushirikiano wa TCRA
na BOT, ” alisema.
Naye Gavana Mkuu wa BOT Profesa Benno Ndulu alisema hadi mwisho wa mwezi
Julai mwaka huu takribani watanzania milioni 21.5 nchi nzima wanatumia
huduma za kifedha kwa njia ya mitandao ya simu.
“Hadi kufikia Julai, 2016 watanzania 21.5 milioni wanatumia mitandao ya
simu walau mara 1 kwa mwezi idadi hii ni kubwa na kwamba inaonesha sekta
hii inakua kwa kasi,” alisema.
Profesa Ndulu alisema kuwa huduma za kifedha kwa njia ya mitandao ya simu imesaidia kukuza uchumi wa nchi.
“Malipo ya fedha kwa njia ya simu yanasaidia kupunguza gharama hivyo na
kuwa kichochea cha maendeleo, sasa hivi wafanyakazi, wakulima,
wanaotumia huduma za bima, wanaonunua bidhaa hulipa kwa Kutumia simu za
mkononi hususani kwamba muda ndio muhimu,” alisema.
Aliongeza kuwa “Mitandao ya simu haiathiri huduma za kibenki, na benki
wamechangamkia kutumia mitandao kufikia wateja wao, hutumia mawakala
kufungulia account, mitandao hii husaidia benki kufikia wateja kote
nchini, woga huo umepungua kwa sasa,”
Tuesday, September 20, 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment